Kanda ya ziwa usipime

created by Tummenye Mwakamba & Upendo Mangula |

English text follow - Hebu fikiria wanaFema kanda nzima mnakutana sehemu moja, unafikiri nini kitatokea hapo? Basi nikwambie, pale Maswa Girls Secondary School, palikuwa hapatoshi, full shangwe, vibe kama lote, vumbi lilikuwa linatimka tu! Moto uliwaka haswaa, hata wasio wanaFema walitamani kujiunga siku hiyohiyo! Upo hapo?!

Si tamasha la kawaida

Hili halikuwa tamasha kama tamasha tu; tamasha letu lilikuwa na kaulimbiu ya “Pinga mimba na ajira za utotoni, okoa nguvukazi ya Taifa.” Tamasha hili liliwakutanisha wanaFema (wanafunzi na walezi) takribani 1,300 kutoka Kanda ya Ziwa. Lengo kuu lilikuwa ni kukumbushana wajibu wetu katika Club, kubadilishana uzoefu, kufahamiana na pia kujenga urafiki miongoni mwa washiriki.

Umoja ndio nguvu yetu

Si mnajua katika Club zetu za Fema tunajifunza vitu mbalimbali na kuna vipaji mbalimbali pia? Basi ule ujuzi wetu na vipaji vyetu hatukuviacha hivihivi, kila mmoja alishiriki hata kwa kujitoa kwa hali na mali ili kufanikisha shughuli tuliyoifanya. Walimu kwa wanafunzi tulishirikiana kuhakikisha mambo yanaenda sawa. Tulipika wenyewe, tulipamba wenyewe na hata burudani zilitolewa na wanaFema wenyewe. Fema Club hatuboi na wala hatupoi!

Hatukukutana bure tu…

Tunaposema vibe kama lote, tunamaanisha. Wana Club walipata wasaa wa kutoa elimu kwa njia ya burudani kupitia nyimbo, mashairi na maigizo. Na ukiachana na hiyo, pia kulikuwa na burudani nyingine kama vile sarakasi, maonesho ya mitindo ya mavazi na vichekesho. Hakuna hata mtu mmoja aliyetoka ukumbini bila kudansi.

Majadiliano ya mustakabali wetu

Pamoja na burudani kulikuwa na wasaa wa kujadiliana kwa lengo la kubadilishana uzoefu na changamoto mbalimbali tunazopitia katika Club zetu, na namna ya kuzitatua. Kulikuwa na makundi 13 ambayo yalipewa maswali manne wayajadili na kuyawasilisha. Ngoja tuwashirikishe nanyi pia;

  • Ni shughuli gani za kipekee ambazo hufanywa na Club yenu?
  • Ni changamoto zipi ambazo huwakumba mnapofanya shughuli hizo?
  • Mafanikio gani mmepata?
  • Mnadhani nini kifanyike kuboresha shughuli hizo?

Baadhi ya mambo yalipatiwa majibu palepale na mengine tukaondoka nayo kama changamoto za kwenda kufanya mabadiliko katika Club zetu.

Wosia wa Mama

Mgeni rasmi alikuwa si mwingine bali mama yetu, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa, Mama Kuyunga Jackson, akimuwakilisha Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Maswa. Alitupatia maneno ya hekima busara; alitaka tuendelee kuzingatia masomo yetu na kuhakikisha tunafanya vizuri darasani kama tunavyofanya kwenye Club zetu. Mbali na hilo hakusita kuweka wazi mapenzi yake juu ya Club za Fema kwa sababu zinawajengea vijana kujiamini kwa maisha ya sasa na kujiandaa kukabiliana na maisha ya baadae.

Picha Nasra Issa Mohamed

Maswa Girls Secondary School Festival

Our festival had the theme "Resist pregnancy and child labor, save the National workforce." The festival brought together about 1,300 Fema (students and guardians) from the Lake Region.The main goal was to remind each other of our responsibilities in the Club, to share experiences, get to know each other and also to build friendships among the participants.

We cooked for ourselves, decorated ourselves and even provided the entertainment. Along with the entertainment there was plenty of discussions with the aim of sharing experiences and challenges we go through in our Clubs, and how to solve them.

Official guest was none other than The Principal of Maswa Girls' Secondary School, Mama Kuyunga Jackson, representing the Maswa District Secondary Education Officer. She gave us words of wisdom and wise; she wants us to continue to focus on our studies and make sure we do as well in the classroom as we do in our Clubs. Besides, she did not hesitate to make clear his passion for Fema Clubs because they build young people's confidence in the present life and prepare them for the future.