Power Talk — Uongo mtupu!

created by Power Teams - Picha K15 Photos |

Mara hili mara lile, mara hiki mara kile. Ni tafrani katika dunia yetu vijana. Huyu anasikia hili, 
naye anamwambia mwingine, nao wanaamini na kuzidi kuyasambaza. Lakini je, umewahi kufuatilia 
ukweli wa hayo unayoyasikia na kuyaamini? Sio uzushi tu? Tena uzushi wa hatari kabisa, 
maana unaleta madhara makubwa sana katika maisha ya watu. Halafu ujue nini…..mambo ya uongo 
huwa yanaenea fastaaaa kama moto nyikani!

* HUU NI MCHEZO WA KUIGIZA NA HAUNA UHUSIANO WOWOTE NA MAISHA HALISI YA WAIGIZAJI. INGAWA ULITUNGWA KUTOKANA NA MATUKIO YA KWELI.

 

Basi, leo Power Team tuko jikoni tunapata zetu chai. Eenh, si unajua mwili haujengwi kwa matofali? Basi kama kawa, huku tunakula, huku ukimya umetawala kidogo; kila mtu yuko bize na simu yake ya kiganjani, huyu anachati, yule anakula muziki, mwingine yuko insta, mara ghafla ...

Mary anaingia jikoni, anachukua kikombe, anakoroga chai.

“Hey Mary, mbona kimya kimya” Hindoo anauliza huku akiwa anakunywa kahawa.
“Amekuwa hivyo tangu amefika leo” Sumaiya anamjibu huku akiingia jikoni.
“Anh, basi tu guys kuna jambo linanivuruga woii” anasema Mary huku akiegemea kabati.
“Jambo gani tena Mary” anauliza Sumaiya, huku akiwa anawasogelea Mary na Hindoo.

Mary huku akiweka kikombe chini “Mmmh, yani acheni. 
Mdogo wangu amepata mimba, halafu anasema aliambiwa akiruka kichurachura baada ya kufanya ngono basi kazi imekwisha, hapati mimba. Yaani kanivuruga, alishindwa hata kuniuliza jamani?!”

“Pole sana Mary, hizi dhana potofu zimekuwa nyingi, zimeenea mno na zinaaminiwa sana” anasema Hindoo kwa masikitiko.
“Na ubaya zaidi ni kwamba hawaulizi, hadi yanawakuta ya kuwakuta” anasema Mary.
“Lakini nyinyi akinadada, kwanini mnaamini hiyo? Au eti mtu anakwambia kwamba mkifanya ngono wakati mmesimama hupati mimba na wewe unakubali jamani?” anauliza Hindoo. 
“Mi naona ni woga wa kuuliza. Watu wanashindwa kutafuta taarifa sahihi ndo kinachotuponza aisee,” anajibu Mary
“Unajua nini, hebu tuziseme zote hizi dhana potofu, leo kaumia mdogo wake Mary, lakini tukiziweka wazi tutasaidia ambao hawajadanganywa,” anasema Sumaiya, “aisee yaani kuna binti mmoja aliambiwa akifanya ngono kwa mara ya kwanza hatapata mimba! Hivi tunavyoongea analea” 

Akadakia Mary “Maskini…..uzushi unatuponza mjue” 

“Tena umenikumbusha, kuna binti mmoja, kadogo tuuu yaani… kamepata mimba juzi juzi tu hapa. Alidanganywa hatopata mimba akifanya ngono kwa sababu hajavunja ungo. Namwoonea huruma jamani” anasema Hindoo.
“Ila haya mambo jamani, hamjawahi kusikia eti ukinywa maji ya baridi baada ya kufanya ngono hupati mimba? Enzi zile tuko shule tulikuwa tunadanganyana kinoma yani,” anasema Mary
“Hata mimi nimewahi kusikia hiyo. Zote uongo mtupu hizo!” anajibu Sumaiya. 
“Em subirini kwanza, eti mtu akifanya mapenzi akiwa hedhi anapata mimba kweli?”Anauliza Hindoo
“Inaweza kutokea. Ujue miili imetofautiana na mizunguko ya hedhi imetofautiana. We jichanganye tu Hindoo. Hahahaaa” akajibu Mary.
“Hahahahaha” wakacheka wote.
“Hata sisi wakaka tunayo yetu ya uongo mjue. Mmesahau ile issue ya kibamia? Eti usipofanya mapenzi muda mrefu uume wako utakuwa mdogo na hutoweza kupata mtoto. Tulikuwa tunachanganyikiwa enzi zile,” anasema Hindo huku akiwa ameegemea kabati.
“Hehehe, achana na hiyo issue kabisa, halafu hamuwezi amini, kuna watu wazima kibao tu wanaamini hiyo issue ni kweli mnajua,” akachangia Sumaiya. 
“Kaaaz kweli kweli” anajibu Hindoo
“Bhana bhana, mi niliambiwa ukiwa na chunusi ni kwa sababu hujafanya ngono. Eti ngono ni tiba ya chunusi” akasema Mary.
“He! He! Hii mpya kwangu, sijawahi sikia kabsaa. Ilinipita!” Anasema Hindoo
“Ndugu mambo ni mengi ohooo. Si mmeona na yaliyompata Shoma kwenye cartoon story yetu ndani ya toleo hili?” anajibu Mary.
“Yeah, nimeona. Masikini Shoma! Angeuliza apate taarifa sahihi yote haya yasingempata,” anasema Sumaiya. 
“Lakini, sio sisi tu tunaodanganywa. 
Hata nyinyi wakaka mnadanganywa, ndo maana mnakuja kutulisha matango pori. Mdogo wangu kalishwa matango pori!” Mary akadakia.
“Daah, pole Mary,” akajibu Hindoo. Jibu lake likafuatiwa na ukimya mkubwa pale jikoni. Baada ya dakika nzima Hindoo akaongeza, “Inabidi kuchunguza taarifa na kupata ukweli kabla ya kumwambia mtu mwingine” akajibu Sumaiya. 
“Guys, me naona kinachofaa zaidi ni kutokufanya ngono na kusubiri mpaka wakati sahihi au mnasemaje?”akauliza Hindoo.
“Hiyo ndo mpango mzima” akajibu Mary
“Na wakati sahihi ukifika, tusisahau kwenda katika kituo cha huduma za afya kupata elimu juu ya afya ya uzazi ili tuwe salama sisi na familia zetu.” Sumaiya anasema huku akimalizia chai yake.
Wakati huo huo simu ya Mary ikaita, “ananipigia mdogo wangu, ngoja nikaongee naye,” akasema Mary huku akielekea mlangoni.