Kuwa na ndoto, ifukuzie, itimize.
By Amabilis Batamula On Nov. 23, 2024
"SHERIA NI CHOMBO CHA KUSAHIHISHA KUTOFAUTIANA KWA KILA AINA."
Dk. Victoria Lihiru alitamani kufundisha, kushauri na kufanya ushawishi wa fikra. Akiwa pale Buzuruga Shule ya Msingi, binti mdogo Victoria Lihiru alitamani tu akikua awe mwalimu ili aisaidie familia yake. Leo, miaka mingi baadaye, anafundisha, lakini sio shule ya msingi. Darasa lake limeenea kuanzia kumbi za Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambako anawajenga kifikra wanafunzi wa chuo kikuu, hadi majukwaa ya kijamii mtandaoni na kwingineko kama vile makongamano na kwenye vyombo vya habari.
Dhamira yake imejikita katika imani kwamba elimu ni nyenzo inayoweza kuleta ulinganifu baina ya watu wa tabaka la chini na la juu, na kwamba sheria ni chombo cha kurekebisha hali ya kukandamizwa kwa makundi fulani. Hili ndilo linalompa nguvu ya kuamka kila siku na azimio thabiti la kushawishi kizazi kipya na kuhamasisha mabadiliko katika mifumo ya utawala ndani na nje ya mipaka. Safari ya Dk. Lihiru inathibitisha nguvu na umuhimu wa kujiamini mwenyewe unapokuwa katikati ya shinikizo za kijamii. “Kama msichana, fahamu kwamba unatosha, ni wa thamani, na unastahili kuwapo—bila maswali wala vikwazo. Nakiwahimiza wasichana kupinga kwa dhana potofu, na kuzipa ndoto zao kipaumbele kuliko matarajio ya jamii.”
Mwaka 2019, Dk. Lihiru alihitimu Shahada ya Uzamivu (Ph.D) katika Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Cape Town, Afrika Kusini. akiwa na umri wa miaka 30. Alipata shahada hiyo miaka si mingi tangu kumaliza shahada yake ya uzamili katika sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Stashahada ya Juu ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo kutoka Shule ya Sheria ya Tanzania, na shahada ya kwanza katika sheria kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Ilikuwa katika mwaka wa pili wa shahada yake ya kwanza ndipo kiu yake ya kushughulikia haki zinazohusiana na uchaguzi na demokrasia ilipobamba. Aliwania nafasi ya rais wa serikali ya wanafunzi Chuo Kikuu Mzumbe, baada ya kuona uwakilishi duni wa wanawake katika vyombo vya maamuzi chuoni hapo. “Tumekuwa tukiona kwamba wanawake na vijana wanakosekana katika nyadhifa za uongozi na maamuzi,” anasema, akiangazia changamoto za kimfumo wanazokutana nazo wanawake na vijana katika nyadhifa za uongozi. “Uongozi mara nyingi huonekana kama jukumu la kiume, jambo ambalo linafanya iwe vigumu kwa wanawake, hasa wanawake vijana, kusikika,” anasisitiza. Katika mchakato huo, alikumbana na ukweli ‘mgumu’ wa upendeleo wa kijinsia katika nyanja za maamuzi.
Hakuchaguliwa, lakini matokeo hayo yakageuka kuwa kichocheo cha kuingia katika harakati za kutetea mabadiliko. Safari yake ikampeleka katika nyanja za kitaaluma, ambapo alichunguza kwa kina mabadiliko ya sheria za uchaguzi, hasa akilenga haki ya kila mtu kuchaguliwa na kushiriki katika nafasi za maamuzi. _“Najitahidi kuona tunakuwa na dunia ambapo wanawake na wanaume, wakiwemo vijana, wana fursa ya kushiriki kwa usawa na haki katika michakato na majukwaa ya maamuzi ya kidemokrasia.” _
Alijihusisha kwa karibu na majukwaa kama vile Women and Constitution Coalition, akitetea usawa wa kijinsia na kushughulikia masuala muhimu kwa haki za wanawake wakati wa mchakato wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2012-2015. Uzoefu huu ulimpeleka kutafuta Ph.D., akilenga kuboresha ushiriki wa wanawake katika michakato ya kikatiba na maamuzi, mada ambayo anaiangazia kwa undani zaidi katika ushirikiano wake wa sasa na Chuo Kikuu cha Pretoria kama postdoctoral researcher. _“Kazi zangu za kitaaluma nimejikita katika kutafiti ni kwa namna gani mifumo ya kisheria ya dola itawezesha wanawake na vijana wengi zaidi kushika nyadhifa za madaraka,” _anatushirikisha. Kutokana na hayo, kazi yake imekuwa na mchango katika mchakato wa marekebisho ya sera na sheria, ikiwa ni pamoja na mazoea na tamaduni za kisiasa, na kuhamasisha umma wa wananchi wa kawaida.
“Sheria ni nyenzo ya kurekebisha ukandamizwaji na ubaguzi wa aina zote,” anasisitiza, akieleza umuhimu wa sheria ya uchaguzi kulijumuisha suala la unyanyasaji wa wanawake katika uchaguzi kama kosa la uchaguzi. Sheria hiyo ilitokana na ushirikiano mkubwa kati ya asasi za kiraia na wabunge. Anauona umuhimu wa kushughulikia mizizi inayosababisha kukosekana kwa usawa wa kijinsia katika michakato ya uchaguzi na ngazi zote za utawala.
Jitihada za Dk. Lihiru zilimpeleka katika majukumu mbalimbali, akipanda ngazi ya taaluma kutoka kuwa Msaidizi wa Mafunzo (Tutoria Assistant) hadi kuwa Mhadhiri Mwandamizi. Pia ana uzoefu mkubwa katika kazi za maendeleo ya kimataifa. Alipata nafasi ya kujitolea na kujifunza katika mashirika kama UN Women, na baadaye akafanya kazi UNDP, ADD International, Palladium Group, Oxfam, na Balozi mbalimbali katika nyadhifa mbalimbali zilizohusu utawala jumuishi na wa kidemokrasia. Kama mshauri elekezi, Dk. Lihiru hutoa ushauri na kufanya utafiti kwa kushirikiana na mashirika ya kijamii, kitaifa, kikanda, na kimataifa kuhusu masuala ya ujumuishi katika utawala wa sheria na wa kidemokrasia, uchaguzi jumuishi, haki za binadamu, masuala ya kikatiba, n.k. Anachangia katika mijadala ya kimataifa, kikanda, na kitaifa kwa kuchapisha matokeo ya tafiti katika machapisho ya kitaaluma na vyombo vya habari vyenye ushawishi mkubwa.
Katika harakati zake, Dk. Lihiru anatambua mchango uliowekwa na washauri(mentors) mbalimbali. Anawashukuru maprofesa Kennedy Gastor, Bernadetha Killian, Alexander Makulilo na wataalamu wa masuala ya jinsia Margaret Rugambwa, na Salome Anyoti, akisema waliichukulia kwa uzito azma yake hiyo na kumuongoza kwenye milango sahihi. Washauri kama Erasmina Massawe walimwonesha njia pale UN Women na katika suala la kushawishi mabadiliko ya kisheria kwa manufaa ya wanawake. “Ni muhimu kusaidia vijana wanapokuwa katika hatua za awali za kujijenga kielimu, kimaarifa, kimtandao, na kikazi.”
Maono ya Dk. Lihiru ni makubwa, ni zaidi ya safari yake ya kibinafsi; anatoa wito kwa vijana kushiriki kikamilifu katika michakato ya kikatiba, kiuchaguzi na kisiasa. “Vijana ndio wengi; wanaweza kutoa mustakabali wa nchi hii," akiwataka vijana kuelekeza nguvu zao katika kushughulikia mapungufu ya kisera na kitaasisi, ambayo yanazuia ushiriki wao.
Akiwa ni Wakili wa Mahakama Kuu na mahakama za chini, Dk. Lihiru anaheshimiwa na wenzake, ni mfano wa kuigwa kwa wanafunzi wake, na ni mtu anayetegemewa miongoni mwa watu wenye maono kama yake. Mama wa watoto wawili, Dk. Lihiru anaufurahia muda wake wa ziada anapokuwa na wanafamilia na marafiki. Japo, anapenda sana kulala, lakini Dk. Lihiru anaamini katika kuamka mapema kama nyenzo ya mafanikio.
Anapenda mazoezi ya kutembea umbali mrefu, kutazama mawio na machweo ya jua, kutazama mawimbi ya bahari, kusikiliza ndege wakiimba, kuangalia bustani, na kusoma.
Read More